Wednesday, 2 November 2016


Simba kuwavaa kiboko wa Yanga


SIMBA, Yanga na Azam zinashuka dimbani leo kwenye viwanja tofauti kwenye michuano ya Ligi Kuu Soka Tanzania bara kila mmoja ikisaka pointi tatu muhimu.

Hata hivyo, mchezo utakaovuta hisia za wapenzi wengi wa michezo ni ule wa Simba na Stand United utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, kwani wapiga debe hao walizikalisha Yanga na Azam FC zilipocheza hapo. Simba ndio kinara ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza michezo 12 na kushinda 10 ikitoka sare mara mbili.

Kwa upande wa Stand United imecheza michezo 13, imeshinda mitano, sare saba na kupoteza mmoja ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 22.

Timu hiyo ya Shinyanga iko vizuri msimu huu na imekuwa ikizishtukiza timu kubwa kwenye Uwanja wa Kambarage, ikijivunia kumchapa Yanga bao 1-0 na Azam FC bao 1-0 na kutamba kuwa hata Simba itakaa chini pia. Iwapo kama kuna timu itafungwa basi yuko hatarini kupitwa na wenzake katika mbio hizo za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo itakuwa na mvutano wa aina yake kwani mashabiki wa soka watataka kuona kama Stand FC itaendeleza ubabe kwa vigogo au ilibahatisha kwa Yanga na Azam tu. Uongozi wa klabu ya soka wa Stand United imeahidi ushindi katika mchezo wao wa leo dhidi ya klabu ya Simba.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Athuman Bilal aliahidi kuwa watapambana kufa au kupona ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Bilal alisema timu yake imejiandaa vyema isipokuwa mshambuliaji wake Abasirim Chidiebele bado majeruhi yanamsumbua.

Mchezaji huyo wa timu ya Pamba fc alisema vijana wake wako safi na ni lazima washinde mchezo huu. Yanga ambao wako katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo atakuwa na mchezo dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Timu hiyo ya Jangwani huenda ikaendelea kupambana kutafuta matokeo mazuri ili kukimbizana na wapinzani wao Simba wanaotesa kileleni.

Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 katika michezo 12, ikishinda minane, sare tatu na kupoteza mmoja. Wametofautiana na wapinzani wao kwa pointi tano.

Mbeya City yenye pointi 16 katika michezo 13 iliyocheza sio timu ya kubeza hasa inapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Sokoine, ambapo amekuwa ikihitaji matokeo.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye uwanja huo Mei mwaka huu, Yanga ilishinda mabao 2-0. Lakini lolote linaweza kutokea kwani huu ni msimu mwingine.

Azam FC itakuwa Mwanza kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba dhidi ya Toto Africans. Timu hiyo ya Chamazi haikuwa vizuri katika michezo kadhaa iliyopita, lakini katika michezo kama miwili iliyopita imeonesha mwanga kuwa inarudi baada ya kushinda.

Azam FC imeshacheza michezo 12, imeshinda mitano, imepata sare nne na kupoteza mitatu hivyo, ikishika nafasi ya nne kwa pointi 19. Toto Africans licha ya kuwa iko vibaya msimu huu baada ya kucheza michezo 13 na kujivunia pointi 11 kwa nafasi ya pili kutoka mwisho, huwa haitabiriki hasa inapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Kila mmoja anahitaji kushinda kujiweka pazuri. Katika mechi hizo hasa kwa Simba, Yanga na Azam FC, wachezaji ambao huenda wakaendeleza rekodi zao za ufungaji ni Shiza Kichuya
wa Simba anayeongoza kwa magoli nane, akifuatiwa na Amis Tambwe wa Yanga mwenye saba na John Bocco wa Azam mwenye magoli sita.

Timu inayoongoza kwa safu bora ya ushambuliaji ni Yanga ikiwa imeshafunga magoli 27 na kufungwa matano, ikifuatiwa na Simba yenye magoli 24 ikifungwa matatu, ikifuatiwa na Azam FC iliyofunga 17 na kuruhusu 11 kupenya kwenye nyavu zao.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni Ndanda FC dhidi ya Tanzania Prisons, Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon na Majimaji dhidi ya JKT Ruvu. Timu hizi kila mmoja anahitaji
ushindi ili kujiweka vizuri, kwani bado wanasaka pointi zaidi ili kufanya vizuri

Wednesday, 26 October 2016







Shein haimiza mikutano ya watendaji kutatua kero
Image result for raisi shein


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ameeleza umuhimu wa viongozi katika Ofisi na Idara za Serikali kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano mara kwa mara na watendaji wao ili kuzungumza na kujadili masuala yao ya kazi.

Dk Shein aliyasema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua matatizo ya watendaji wao pamoja na kukaa kwa pamoja kwa lengo la kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo kwa haraka na hatimae kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalumu kati yake na uongozi wa Ofisi ya Rais, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati ilipowasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017 ya ofisi hiyo.

Katika maelezo yake, alisema ni jukumu kwa kila mkuu wa Idara kuwa na utaratibu huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kupata maamuzi ya haraka sambamba na kuweza kufanya kazi kwa pamoja hatua ambayo pia, hupunguza mivutano na hujenga mafahamiano makubwa.

Aidha, alieleza kuwa kukaa pamoja kati ya kiongozi na watendaji wake kunasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia muwafaka katika kujadili masuala mbali mbali ya kiutendaji hali ambayo huzidisha mshikamano na kujenga udugu miongoni mwao.

Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utendaji wao wa kazi sambamba na kazi nzuri ya uwasilishaji na utekelezaji wa Mpango Kazi uliofanywa na Ofisi hiyo.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu akisoma taarifa ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo, na kusema kuwa Ofisi ya Rais imedhamiria kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili waishi kwa amani, mshikamano na upendo miongoni mwao