Shein haimiza mikutano ya watendaji kutatua kero
Dk Shein aliyasema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua matatizo ya watendaji wao pamoja na kukaa kwa pamoja kwa lengo la kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo kwa haraka na hatimae kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalumu kati yake na uongozi wa Ofisi ya Rais, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati ilipowasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017 ya ofisi hiyo.
Katika maelezo yake, alisema ni jukumu kwa kila mkuu wa Idara kuwa na utaratibu huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kupata maamuzi ya haraka sambamba na kuweza kufanya kazi kwa pamoja hatua ambayo pia, hupunguza mivutano na hujenga mafahamiano makubwa.
Aidha, alieleza kuwa kukaa pamoja kati ya kiongozi na watendaji wake kunasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia muwafaka katika kujadili masuala mbali mbali ya kiutendaji hali ambayo huzidisha mshikamano na kujenga udugu miongoni mwao.
Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utendaji wao wa kazi sambamba na kazi nzuri ya uwasilishaji na utekelezaji wa Mpango Kazi uliofanywa na Ofisi hiyo.
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu akisoma taarifa ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo, na kusema kuwa Ofisi ya Rais imedhamiria kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili waishi kwa amani, mshikamano na upendo miongoni mwao
No comments:
Post a Comment